Swahili New Testament Bible

1st Timothy 4

1 Timothy

Return to Index

Chapter 5

1

 Usimkemee mtu mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana kama ndugu zako, 

2

 wanawake wazee kama mama yako, na wasichana kama dada zako, kwa usafi wote. 

3

 Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli. 

4

 Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu. 

5

 Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana. 

6

 Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai. 

7

 Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama. 

8

 Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini. 

9

 Usimtie katika orodha ya wajane, mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu, 

10

 na awe mwenye sifa nzuri: aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema. 

11

 Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo watataka kuolewa tena, 

12

 na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali. 

13

 Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema. 

14

 Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili adui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu. 

15

 Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani. 

16

 Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachilia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa. 

17

 Wazee wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha. 

18

 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Usimfunge ng`ombe kinywa anapopura nafaka." na tena "Mfanyakazi astahili malipo yake." 

19

 Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu. 

20

 Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa. 

21

 Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu, na mbele ya malaika watakatifu uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda. 

22

 Usiharakishe kumwekea mtu yeyote mikono kwa ajili ya kumtumikia Bwana. Usishiriki dhambi za wengine; jiweke katika hali safi. 

23

 Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara. 

24

 Dhambi za watu wengine huonekana waziwazi, nazo zawatangulia kwenye hukumu; lakini dhambi za wengine huonekana tu baadaye. 

25

 Vivyo hivyo, matendo mema huonekana waziwazi, na hata yale ambayo si dhahiri hayawezi kufichika. 

1st Timothy 6

 

 

 

Please Click the Ads.

Clicking the Ads helps us to keep this free Bible website open for everyone.

Thanks!

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: